JEWAJUA
Kisiwa cha midoli (Isla de las Munecas) kinachopatikana jiji la Mexico, Xochimilco, ni mojawapo ya mahala maarufu paogofu juu ya uso wa dunia. Ni mahala ambapo raia yeyote wa Mexico hujiuliza mara mbilimbili kabla ya kwenda huko, na si tu wao, bali mtu yeyote mwenye taarifa na eneo hilo kutokana na simulizi zake ambazo husisimua vinyweleo.
Huko, kisiwani, kwenye matawi na miti iliyokufa, inaning’inia mamia ya midoli: iliyoumbwa katika njia ambayo inatisha. Midoli hiyo inaaminika kuwa na vituko ambavyo huhisiwa ama kusikika punde pale watazamaji wanapovigeuzia visogo.
Simulizi hii inaanzia huko nusu karne iliyopita, kipindi hicho msichana mdogo alizama majini na inasemekana akatuama kwenye mifereji ya kina inayopatikana eneo hilo la Xochimico.
Baadae kisiwa hicho kilikuja kukaliwa na mwanaume aendaye kwa jina la Don Juian Santana Barrera, ambaye japokuwa alikuwa na familia, aliamua kwenda kuishi kwenye kisiwa hicho peke yake.
Muda fulani wakati Barrera akiwa anavua baharini, inasemekana eneo lile lile ambapo mwili wa yule binti ulituama, akajikuta akimvua mdoli (mwanasesere) mmoja. Kitendo hicho hakikukoma baada ya mara moja tu, mwanaume huyo, Barrera, akawa anavua mdoli mmoja baada ya mwingine.
Hili jambo lilimshtusha sana, na ilitokea akaamini ilikuwa ni ishara ya roho ya kishetani, hivyo basi kuiridhisha na kutuliza roho hiyo isimdhuru akawa anatundika midoli hiyo kisiwani. Mwishowe alijikuta amejaza midoli mingi mno. Midoli hiyo ilikuwa na kasoro kadha wa kadha kwenye maungo mathalani macho mabovu yanayotisha, miguu na mikono iliyonyofoka.
Bwana Santanna Barrera hakufanya juhudi yoyote kuitengeneza midoli hiyo, kwa namna alivyokuwa anaiokota ndivyo alivyokuwa anaiweka.
Watu wengi waliokuja hapo kisiwani wakatishwa sana na midoli hiyo, lakini yeye, mwenyeji, alionekana akiwa huru pasipo kughasiwa na vitu hivyo. Kwa furaha kubwa alikuwa anawadadavulia wageniwe ni kwa namna gani ameweza kurandana na ulimwengu wa roho.
Aliishi hapo kisiwani kwa miaka hamsini kabla ya kifo kumtwaa mwaka 2001. Ajabu ni kwamba mwili wake ulikuja kupatikana eneo lile lile ambapo binti yule mdogo alipofia.
Inaaminika roho ya Barrera imeungana na ya yule binti mdogo, na ni wao sasa ndio wanausumbua ndani ya kisiwa hicho. Wageni na watalii kadhaa husema wanasikia sauti ya kunong’ona toka kwenye midoli hiyo wakati wa usiku, na hata kuona macho ya wanasesere hao yakisogea kutoka upande mmoja kwenda mwingine kuwafuata.
Barrera, kipindi yupo hai kisiwani, alidai alikuwa anasikia sauti za vishindo vya miguu na hata minong’ono japokuwa alikuwa maili kadhaa mbali toka kwenye mchangamano wa watu Mexico city. Na kutokana na hivyo basi, Barrera akawa ametia juhudi zake kwenye kuanika midoli ili basi apoze roho hiyo iliyokuwa inasumbua.
Ni miaka kumi na 17 sasa tangu Barrera afariki. Midoli yake aliyoipachika haijaguswa kabisa. Na hata baadhi ya wageni wengine wanaokuja hapo huongezea midoli mipya hapo.
Wengine huamini binti huyo mdogo hakuwahi kutokea, bali tu ni taswira za Barrera baada ya kukaa huko msituni mwenyewe.
Lakini maswali yanabaki kwamba, midoli ile Barrera aliyokuwa anaivua sehemu moja ilikuwa inatokea wapi? Na je kuna namna gani Barrera alikuja kufia papo hapo? Nini kinachotosha kuelezea mawazo ya watalii wafikao hapo ambao nao husema kile kile ambacho Barrera aliwahi kukisema – kusikia minong’ono na hatua za watu?
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Comment yako ni muhimu sana