Jumanne, 2 Januari 2018

Miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito, (first trimester) huwa na mabadiliko mbalimbali kimwili na kisaikolojia yanayotoka na homoni za uzazi kuzalishwa kwa wingi zaidi. Mabadiliko haya hutofautiana kati ya mwanamke na mwanamke, na pia kwa mwanamke mmoja kwa nyakati tofauti.
Kipindi hiki mjamzito huweza kupata mabadiliko yafuatayo ambayo huwa pia kama dalili za mwanzo za ujauzito;

1.Kutokwa damu kidogo (matone kwenye nguo za ndani) kwa siku moja au mbili.
Hii inaweza kutokea kwa baadhi ya wanawake kutokana na kiinitete (embryo) kujipandikiza katika mji wa uzazi. Ni ya muda mfupi na damu hutoka kidogo sana, na pia hutokea kwa baadhi ya wanawake.

2.Hali ya Kuchoka Haraka Zaidi ya Kawaida.
Katika kipindi hiki cha mwanzo cha ujauzito, mwanamke anaweza kupata hali ya uchovu mara kwa mara. Na hii inaweza kuwa uchovu wa kawaida au kuchoka sana zaidi ya kawaida (ukilinganisha na kipindi ambacho hakuwa na ujauzito).

3.Kutapika hasa Wakati wa Asubuhi (morning sickness).
Hii ni hali ya kawaida kwa wanawake wengi wakati wa mwanzo wa ujauzito, na hupungua kadri mimba inavyokuwa. Ikiwa unatapika sana karibu siku nzima kila kitu unachokula onana na daktari mapema.

4.Kukojoa Mara kwa Mara.
Tumbo la uzazi huanza kukua na kukandamiza kibofu cha mkojo na hivyo kuleta hali ya kukojoa mara kwa mara.

5.Kukosa Hamu kwa Baadhi ya Vyakula
Kutopenda baadhi ya vyakula, vinywaji na baadhi ya harufu natokea mara nyingi kutokana na mabadiliko ya kihomoni mwiIini.

6.Kununa na Kukasirika (mood changes).
Hizi moods hubadilika mara kwa mara wakati mwingine .furaha, uchangamfu, na wengine inakuwa ni rahisi sana kumchukiza hata kwa kitu kidogo. Kuna wajawazito wengine hutokea kuwachukia wenzi wao pia. Hivyo ni muhimu kuwachukulia katika hilo.

7. Matiti Kuvimba na Kuuma
Mara nyingi mabadiliko ya kihomoni huchangia kuleta hali hii. Polepole matiti huanza kukua kujiandaa kutengeneza maziwa kwa ajili ya mtoto, mabadiliko haya huchangia kuleta hali ya matiti kuvimba na kuuma.

8. Mabadiliko katika Hamu ya Kufanya Mapenzi.
Na hili pia hutokea, ikitofautiana kati ya wakati na wakati. Kuna wajawazito au wakati mjamzito anakuwa na mihemko mikubwa ya kimapenzi na wakati mwingine inakuwa kinyume kabisa. Ingawa inaweza isiwe kwa kiasi kikubwa katika miezi hii 3 ya mwanzoni.

9. Mabadiliko ya Ngozi
Ingawa inaweza isikupate, mabadiliko ya ngozi hutokea hasa kutokana na mabadiliko ya kihomoni mwilini. Chunusi huweza kutokea.

10. Kukosa Hedhi
Ni ishara mojawapo kuu ya ujauzito, kwa kawaida haitegemewi mwanamke mjamzito kuendelea kupata siku zake za hedhi isipokuwa kuotokwa na damu kidogo (matone kidogo kwenye nguo za ndani kwa siku moja au mbili). Kupata hedhi ya kawaida au kutokwa damu nyingi wakati wa ujauzito huashiria hatari ya ujauzito kutoka, hivyo ni muhimu kwenda hospitali mapema.

Mabadiliko haya hutofautiana kati ya mwanamke na mwanamke, hata siku kwa siku. Ukipata dalili zozote zinazokupa wasiwasi, onana na daktari wako haraka.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Comment yako ni muhimu sana